Friday, January 22, 2010
Tishio la Majembe Dawasco lakusanya bil. 8/- kwa wiki
SIKU sita baada ya kampuni ya Majembe Auction Mart kutangaza kuanza operesheni ya kukata maji na kukusanya madeni ya Mamlaka ya Maji Dar es Salaam (DAWASCO), baadhi ya wateja waliokuwa wakidaiwa wamelipa sh. bilioni nane na kupunguza deni la awali kutoka sh. bilioni 28 hadi sh. bilioni 20.
Alhamisi iliyopita, kampuni ya Majembe maarufu kama Vijana wa Kazi, walitangaza operesheni ambayo ingeanza jana Dar es Salaamu, na kabla ya kuanza kwake wadaiwa wengi sugu walimiminika Dawasco na kulipa zaidi ya Sh bilioni nane.
Katika siku ya kwanza ya operesheni hiyo itakayodumu kwa mwezi mmoja, nyumba sita zilikatiwa maji na Mkurugenzi Mtendaji wa Majembe, Bw. Sett Motto alisema kuwa walengwa ni wateja waliojiunganishia maji na wadaiwa sugu ambao watakatiwa maji.
"Kwa leo tunataka wananchi wajue kuwa zoezi lipo na ni endelevu, tumeanza kwa nyumba chache na leo tuapita nyumba kwa nyumba ili kubaini wanaotumia maji bila kulipa," alisema Bw.Motto
Bw. Motto alisema wananchi watakaowafichua waliojiunganishia maji watapewa zawadi ya sh. 5,000,000,ambapo kwa wadaiwa sugu watakaojitokeza kulipa bili zao watapunguziwa kiasi kidogo.
Aidha alisema kwamba lengo la kufanya hivyo ni kuipunguzia madeni DAWASCO kutokana na wengi kushindwa kulipa bili kwa wakati, hivyo kulifanya shirika hilo kuingia hasara kubwa.
Ofisa Uhusiano wa DAWASCO, Bi. Mary Lyimo alisema kuwa wateja wengi wamekuwa na tabia ya kukaa kwa muda mrefu bila kulipa madeni na kusababisha kukosekana kwa matengenezo ya baadhi ya miundombinu nchini.
"Wateja 4,000 ni wadaiwa sugu, wengi wao wanadaiwa milioni 1 na kuendelea, hii inatupa sana tabu katika ufatiliaji lakini tunaamini majembe watatusaidia zaidi katika operesheni hii," alisema Bi. Lyimo
Baadhi ya wadaiwa sugu waliokatiwa maji jana ni pamoja na Bw. Makua Chombo mtaa wa Elikoma Kariakoo anayedaiwa sh 1,458,000, kampuni ya Fazal Communication (Sofia House) iliyopo Livingstone Kariakoo inayodaiwa sh. 2,445,964 na Bw. Juma Salim wa Mtaa wa Udoe Kariakoo anayedaiwa Sh. 1,016,800.
Subscribe to:
Posts (Atom)