Katika kuimarisha usimamizi wa utoaji huduma za usafiri na kuondoa kero kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam,Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Mjini(SUMATRA) imeteua Kampuni ya Majembe Auction Mart kuwa wakala wake wa kufuatilia utekelezaji wa masharti ya leseni ya usafirishaji abiria kwa mabasi yanayotoa huduma ya usafiri katika Mkoa wa Dar es Salaam(Daladala)na pia mabasi ya Mikoani yanayoanzia Kituo Kikuu cha Ubungo.
Kampuni ya Majembe Auction Mart ambayo imeteuliwa kufanya kazi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja itatekeleza majukumu waliyopewa kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani.
Moja ya majukumu makubwa ya Kampuni hiyo itakuwa ni kusimamia na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa mabasi ya Daladala yanayotoa huduma katika Jiji la Dar es Salaam na viunga vyake ili kuhakikisha kuwa masharti ya leseni ya usafirishaji abiria yanafuatwa na watoa huduma ili hatimaye huduma ya usafiri katika Jiji iwe bora na yenye kukidhi mahitaji na matarajio ya wakazi wa Dar es Salaam.
Ili huduma ya usafiri katika Jiji iendelee kuwa bora zaidi,ni matarajio ya Mamlaka kuwa wamiliki,madereva pamoja na makondakta wa mabasi ya Daladala watatoa ushirikiano unaostahili kwa Majembe Auction Mart na Kikosi cha Usalama Barabarani wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.Aidha wadau na wananchi kwa ujumla wanaombwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa mamlaka zinazosimamia usafiri pamoja na Kampuni ya Majembe kwa lengo la kuimarisha usimamizi na kuboresha huduma hii muhimu kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.
Mamlaka ya SUMATRA itafuatilia na kusimamia kwa karibu sana utendaji wa wakala Majembe Auction Mart kwa mujibu wa Sheria na Taratibu ili kuondoa kero za usafiri kwa wakazi wa Dar es Salaam.Tuchukue fursa hii pia kuwakumbusha wananchi kupunguza purukushani kwa kupanga mstari wakati wa kupanda mabasi.
No comments:
Post a Comment